Isaiah 34

Hukumu Dhidi Ya Mataifa


1 aNjooni karibu, enyi mataifa, nanyi msikilize;
sikilizeni kwa makini,
enyi kabila za watu!
Dunia na isikie, navyo vyote vilivyo ndani yake,
ulimwengu na vyote vitokavyo ndani yake!

2 b Bwana ameyakasirikia mataifa yote;
ghadhabu yake ni juu ya majeshi yao yote.
Atawaangamiza kabisa,
atawatia mikononi mwa wachinjaji.

3 cWaliouawa watatupwa nje,
maiti zao zitatoa uvundo,
milima itatota kwa damu zao.

4 dNyota zote za mbinguni zitayeyuka
na anga litasokotwa kama kitabu,
jeshi lote la angani litaanguka
kama majani yaliyonyauka kutoka kwenye mzabibu,
kama tini iliyonyauka kutoka kwenye mtini.


5 eUpanga wangu umekunywa na kushiba huko mbinguni,
tazama, unashuka katika hukumu juu ya Edomu,
wale watu ambao nimeshawahukumu,
kuwaangamiza kabisa.

6 fUpanga wa Bwana umeoga katika damu,
umefunikwa na mafuta ya nyama:
damu ya kondoo na mbuzi,
mafuta kutoka figo za kondoo dume.
Kwa maana Bwana ana dhabihu huko Bosra,
na machinjo makuu huko Edomu.

7 gNyati wataanguka pamoja nao,
ndama waume na mafahali wakubwa.
Nchi yao italowana kwa damu,
nayo mavumbi yataloa mafuta ya nyama.


8 hKwa sababu Bwana anayo siku ya kulipiza kisasi,
mwaka wa malipo,
siku ya kushindania shauri la Sayuni.

9 iVijito vya Edomu vitageuka kuwa lami,
mavumbi yake yatakuwa kiberiti kiunguzacho,
nchi yake itakuwa lami iwakayo!

10 jHaitazimishwa usiku wala mchana,
moshi wake utapaa juu milele.
Kutoka kizazi hadi kizazi itakuwa ukiwa,
hakuna mtu yeyote atakayepita huko tena.

11 kBundi wa jangwani na bundi mwenye sauti nyembamba wataimiliki,
bundi wakubwa na kunguru wataweka viota humo.
Mungu atanyoosha juu ya Edomu
kamba ya kupimia ya machafuko matupu,
na timazi ya ukiwa.

12 lWatu wake wa kuheshimiwa hawatakuwa na chochote
kitakachoitwa ufalme huko,
nao wakuu wao wote watatoweka.

13 mMiiba itaenea katika ngome za ndani,
viwawi na michongoma itaota
kwenye ngome zake.
Itakuwa maskani ya mbweha,
makao ya bundi.

14 nViumbe vya jangwani vitakutana na fisi,
nao mbuzi-mwitu watalia wakiitana;
huko viumbe vya usiku vitastarehe pia
na kujitafutia mahali pa kupumzika.

15 oBundi wataweka viota huko na kutaga mayai,
atayaangua na kutunza makinda yake
chini ya uvuli wa mabawa yake;
pia huko vipanga watakusanyika,
kila mmoja na mwenzi wake.

16 pAngalieni katika gombo la Bwana na msome: Hakuna hata mmoja katika hawa atakayekosekana,
hakuna hata mmoja atakayemkosa mwenzi wake.
Kwa kuwa ni kinywa chake Mungu kimeagiza,
na Roho wake atawakusanya pamoja.

17 qHuwagawia sehemu zao,
mkono wake huwagawanyia kwa kipimo.
Wataimiliki hata milele
na kuishi humo kutoka kizazi hadi kizazi.
Copyright information for SwhKC